Friday, September 09, 2022

NUKTA AFRIKA,UNESCO YATAJA FAIDA YA WANAHABARI KUJIFUNZA

 


Mkufunzi wa Nukta Africa Nuzulack Dausen akifundisha wanahabari  ambao hawapo picha katika moja ya mafunzo kuhusu habari za takwimu jijini Arusha 2021. Picha Maktaba



Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wametaja faida mbalimbali kwa wanahabari nchin,i kupata mafunzo maalum yatakayosaidia kuboresha maudhui yanayozalishwa na vyombo vya habari Tanzania.

Nukta Africa na UNESCO kuwa na  programu ya miezi mitatu itakayowakutanisha  wahariri na waandishi wa habari kujengewa uwezo katika maeneo makuu matatu ya uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji habari na “multimedia storytelling”.

Miongoni mwa faida ambazo zimetajwa ni kuwa na ujuzi wa kung'amua habari za uzushi na kweli, kuepuka kusambaza uzushi na kuathiri wengine pamoja kujifunza zana za kijidigitali za kubaini 'mafamba' kama picha & video za uzushi, Mafunzo hayo yatakayoanza mwishoni mwa Septemba 2022 yatatolewa kwa njia ya mtandao kutoka kwa wakufunzi waliobobea katika tasnia ya habari Tanzania na duniani.

Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano UNESCO Dar es salaam, Nancy Angulo  amesema programu hiyo imelenga kushirikisha na kuwafahamisha watunga sera, taasisi za vyombo vya habari na washirika wa maendeleo namna ya kuboresha maslahi ya vyombo vya habari nchini Tanzania.

“Ni muhimu kuimarisha mikakati na uhamasishaji wa namna ya upatikanaji wa rasilimali kwa vyombo vya habari na waandishi ili kuwepo na maslahi  uendelevu katika tasnia ya habari,” amesema Angulo. 

Mafunzo hayo yatatolewa katika awamu tatu na jumla ya washiriki 100 watafaidika na programu hiyo ili kuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa kupitia maudhui yenye ubora na yenye kugusa maisha ya watu.

Mafunzo hayo ni moja ya mipango ya UNESCO chini ya Programu ya Kimataifa ya Maendeleo katika Mawasiliano (International Programme for the Development of Communication) yenye lengo la kuwezesha wanahabari na vyombo vya habari katika nchi zinazoendelea kuwa na uwezo wa kujitegemea.

Daniel Mwingira, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo wa Nukta Africa amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanahabari nchini Tanzania kwa sababu watapata mbinu mpya hasa za kidijitali kuwawezesha kuzalisha habari zenye ubora wa hali ya juu.

“Dunia inaenda kwa kasi na Tanzania siyo kisiwa hivyo wanahabari wanapaswa kupata maarifa mapya ili waweze kuboresha habari zao na kuandika habari zenye manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Mwingira.

Aidha Mwingira amesema wanatarajia kuwafundisha wanahabari habari za takwimu, namna ya kuthibitisha taarifa pamoja na mbinu mpya za kuandika habari kwa mfumo wa kisasa.

Mwanandishi wa habari anayechipukia, Lucy Samson akihojiwa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati mwafaka ili kuwasaidia waandishi habari kuongeza maarifa na ufanisi katika kazi zao za kila siku.

“Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hivyo waandishi wa habari tunapaswa kuwa na ujuzi ili kwenda na wakati hivyo mafunzo haya yatasaidia sana waandishi wa habari,” amesema Samson.

Ili kupata fursa ya kuwa miongoni mwa watu watakaopata mafunzo haya, hakikisha unatuma maombi yako kupitia kiunganishi hiki >>>> bit.ly/3CDA3jW.

0 komentar:

Post a Comment