Friday, September 09, 2022

Rais Samia Asaini Kitabu Cha Maombolezo Kifo Cha Malkia Elizabeth II Wa Uingereza, Oysterbay Jijini Dar Es Salaam

 




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Malkia Elizabeth II (96) wa Uingereza aliyefariki tarehe 08 Septemba, 2022 nchini Uskochi. Mhe. Rais Samia alisaini Kitabu hicho katika Makazi ya Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Oysterbay Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2022.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar mara baada ya kusaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Malkia Elizabeth II (96) wa Uingereza aliyefariki tarehe 08 Septemba, 2022 nchini Uskochi.

NUKTA AFRIKA,UNESCO YATAJA FAIDA YA WANAHABARI KUJIFUNZA

 


Mkufunzi wa Nukta Africa Nuzulack Dausen akifundisha wanahabari  ambao hawapo picha katika moja ya mafunzo kuhusu habari za takwimu jijini Arusha 2021. Picha Maktaba



Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wametaja faida mbalimbali kwa wanahabari nchin,i kupata mafunzo maalum yatakayosaidia kuboresha maudhui yanayozalishwa na vyombo vya habari Tanzania.

Nukta Africa na UNESCO kuwa na  programu ya miezi mitatu itakayowakutanisha  wahariri na waandishi wa habari kujengewa uwezo katika maeneo makuu matatu ya uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji habari na “multimedia storytelling”.

Miongoni mwa faida ambazo zimetajwa ni kuwa na ujuzi wa kung'amua habari za uzushi na kweli, kuepuka kusambaza uzushi na kuathiri wengine pamoja kujifunza zana za kijidigitali za kubaini 'mafamba' kama picha & video za uzushi, Mafunzo hayo yatakayoanza mwishoni mwa Septemba 2022 yatatolewa kwa njia ya mtandao kutoka kwa wakufunzi waliobobea katika tasnia ya habari Tanzania na duniani.

Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano UNESCO Dar es salaam, Nancy Angulo  amesema programu hiyo imelenga kushirikisha na kuwafahamisha watunga sera, taasisi za vyombo vya habari na washirika wa maendeleo namna ya kuboresha maslahi ya vyombo vya habari nchini Tanzania.

“Ni muhimu kuimarisha mikakati na uhamasishaji wa namna ya upatikanaji wa rasilimali kwa vyombo vya habari na waandishi ili kuwepo na maslahi  uendelevu katika tasnia ya habari,” amesema Angulo. 

Mafunzo hayo yatatolewa katika awamu tatu na jumla ya washiriki 100 watafaidika na programu hiyo ili kuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa kupitia maudhui yenye ubora na yenye kugusa maisha ya watu.

Mafunzo hayo ni moja ya mipango ya UNESCO chini ya Programu ya Kimataifa ya Maendeleo katika Mawasiliano (International Programme for the Development of Communication) yenye lengo la kuwezesha wanahabari na vyombo vya habari katika nchi zinazoendelea kuwa na uwezo wa kujitegemea.

Daniel Mwingira, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo wa Nukta Africa amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanahabari nchini Tanzania kwa sababu watapata mbinu mpya hasa za kidijitali kuwawezesha kuzalisha habari zenye ubora wa hali ya juu.

“Dunia inaenda kwa kasi na Tanzania siyo kisiwa hivyo wanahabari wanapaswa kupata maarifa mapya ili waweze kuboresha habari zao na kuandika habari zenye manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Mwingira.

Aidha Mwingira amesema wanatarajia kuwafundisha wanahabari habari za takwimu, namna ya kuthibitisha taarifa pamoja na mbinu mpya za kuandika habari kwa mfumo wa kisasa.

Mwanandishi wa habari anayechipukia, Lucy Samson akihojiwa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati mwafaka ili kuwasaidia waandishi habari kuongeza maarifa na ufanisi katika kazi zao za kila siku.

“Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hivyo waandishi wa habari tunapaswa kuwa na ujuzi ili kwenda na wakati hivyo mafunzo haya yatasaidia sana waandishi wa habari,” amesema Samson.

Ili kupata fursa ya kuwa miongoni mwa watu watakaopata mafunzo haya, hakikisha unatuma maombi yako kupitia kiunganishi hiki >>>> bit.ly/3CDA3jW.

AUDIOMACK YAZINDUA 'NGOMA JUA YA NGOMA' KUKUZA UBUNIFU, MUZIKI WA KITANZANIA

 KAMPUNI  ya Audiomack imezindua kampeni inayojulikana  “Ngoma Juu Ya Ngoma” inayolenga kukuza ubunifu na kuuza muziki wa Kitanzania na itashirikisha wasanii wakubwa wakiwemo Zuchu, Lava Lava, Jux, Barnaba na wengine.

Kampeni itahusisha Bango, ushirikiano wa Radio na, matangazo ya kidijitali, chapa ya mabasi, ushiriki wa watu wenye ushawishi na orodha za kucheza.

Katika kukuza uelewa juu ya kampeni hiyo Audiomack  ilifanya Warsha Katika jiji la Dar es Salaam hivi karibuni.

Kampeni hiyo pia itahusisha mfululizo wa kwanza wamuziki wa kimataifa wa Audiomack, SKYLINE, mfululizo wamaonyesho unaohusisha matukio yaliiyotajwa hapo juu,  na utaonyesha tamaduni kutoka Tanzania nakuziweka katika ubora wa juu zaidi ambao maudhui  ya Audiomack yanajulikana nayo.

Audio mack pia imeshirikiana na kituo cha redio cha msanii Diamond Platnumz kilichoshinda tuzoz a Tanzania Wasafi FM kuzindua ‘Audiomack Top 10’.

Kipindi hicho kinachorushwa Ijumaa, kinaundwa na chati za Audiomack Top 10 Tanzania zinazoangazia nyimbo kubwa zaidin chini.


WADAU WA ELIMU WAWEKA BAYANA UMUHIMU WA MAKTABA MAADHIMISHO SIKU YA USOMAJI

 

Mkurugenzi Idara ya Ubunifu na Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Bw. Fixon Mtelesi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bw. Juvenalius Kuruletera akizugumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani lililofanyika jijini Dar es Salaam na kushirikisha baadhi ya wadau wa elimu nchini.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo wakishiriki katika mjadala.
Mkufunzi Mwandamizi wa Usomaji na Maktaba, Room to Read, Bi. Eva Sanga akizungumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki kwenye hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.

Na Mwandishi Wetu, Dar
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo kukuza stadi za usomaji kwa wanafunzi hasa wa shule za msingi ili kuwaongezea uelewa na uwezo wa kuyamudu masomo yao.

Kauli hiyo imetolewa na jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Idara ya Ubunifu na Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) , Bw. Fixon Mtelesi alipozungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.

Akizungumza Bw. Mtelesi alisema kumjengea mwanafunzi utamaduni wa kupenda kujisomea kunakuza stadi na kumuongezea uelewa wa kumudu masomo yake mengine na kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema TIE inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuboresha elimu kwa ngazi zote, hasa uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, vyoo na ukarabati wa shule mbalimbali; hivyo kuiomba pia kuangalia suala zima la uanzishwaji wa maktaba kwa shule za msingi kwa kuwa ni kitovu cha maarifa katika ujifunzaji.

"..Kama tunavyofahamu kuwa kujenga utamaduni usomaji imekuwa mada na lengo la muda mrefu la nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania. Hata hivyo licha ya jitihada hizo zinazochuliwa na mataifa katika kukuza usomaji, tafiti zinaonesha kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu duniani wasiojua kusoma vizuri na wasiokuwa na tabia ya usomaji," alisema Bw. Mtelezi katika kongamano hilo lililobeba kauli mbiu; 'Uboreshaji wa Mazingira ya Usomaji na Ujifunzaji'.

Naye, Mkurugenzi wa Mradi wa Usomaji na Maktaba Room to Read Tanzania, Bw. Joachim Kahwa akizungumza katika kongamano hilo, alisema wanaamini kuwa maktaba ndio sehemu pekee ambayo mtoto huweza kupata fursa ya kuendeleza stadi za kusoma na kujenga tabia ya usomaji.

Room to Read humsaidia katika kujenga msingi bora wa kumudu stadi za kusoma na kuandika katika darasa la kwanza na la pili ili kujua kusoma kwa wakati, kisha, kutumia stadi hizo kujisomea maktaba ili kujenga tabia ya usomaji ili kujifunza zaidi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mtoto mwenye tabia ya usomaji hupenda kusoma kwa hiari mara kwa mara na hufurahia usomaji. ili kumvutia mtoto kujenga tabia ya usomaji Room to Read tunahamasisha uwepo wa maktaba zenye vitabu vya hadithi vilivyoandaliwa vizuri, vyenye kuvutia, vilivyopangiliwa kwa ngazi kulingana na uwezo wa usomaji wa watoto na mazingira rafiki kwa mtoto," alisisitiza, Bw. Kahwa.

Maadhimiso ya Siku ya Usomaji Duniani hufanyika kila mwaka Septemba 8 ikiwa ni matokeo ya tamko la Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (UNESCO) lililotolewa tarehe 26 Oktoba 1966.

Wednesday, February 09, 2022

Rais Samia Suluhu amuapisha Mhe. Angeline Mabula kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

 


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Angeline Mabula kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 09 Februari, 2022

Rais Wa Benki Ya AADB Ahaidi Neema Kwa Tanzania

 


Na Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuahidi kutekeleza miradi mipya katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na pia kuwawezesha Wanawake na Vijana kiuchumi  pamoja na ahadi aliyoitoa ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR

Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki hiyo, Dkt. Akinwumi Adesina, akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.

Alisema kuwa Benki hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko za jijini Dodoma pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Msalato utakaojengwa mkoani Dodoma, miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amemshukuru Rais huyo wa Benki ya AfDB kwa nia ya kusaidia miradi mingine mipya kama ya Uwezeshaji wa Wanawake na vijana lakini pia uwezeshaji katika sekta kuu za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo.

Amesema maeneo hayo ni muhimu katika kukuza uchumi na yanamatokeo chanya si tu kwa watanzania lakini pia kwa Bara la Afrika kwa kuwa mradi kama wa Reli utazinufaisha nchi Jirani kwa kuwa Tanzania ina lango la Bahari hivyo miundombinu hiyo itasaidia katika kuchochea uchumi wa nchi hizo Jirani na nyingine.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameipongeza Benki hiyo kwa utendaji kazi mahili chini ya Rais Dkt. Akinwumi Adesina, kwa kuwa mwaka 2021 ilitunukiwa tuzo kwa kuwa Benki Bora Duniani katika masuala ya Fedha na pia ameshukuru kwa nia ya kusaidia utekelezaji wa miradi mipya ambayo itawasaidia watanzania.

Kwa upande wake Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina alisema kuwa Benki yake inatambua umahili wa Tanzania katika kusimamia sera za kifedha na kiuchumi na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuchangia maendeleo yake katika Nyanja mbalmbai ikiwemo miundombinu ya nishati na barabara, kilimo, uhifadhi wa mazingira, pamoja na kuendeleza sekta binafsi.

Dkt. Adesina alisema kuwa uwekezaji wa Benki yake katika miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi hapa nchini umefikia dola za kimarekani bilioni 2.5 na kwamba Benki yake iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya hususani katika sekta ya kilimo ili nchi iweze kuzalisha chakula kwa wingi na kukiongezea thamani kupitia maeneo maalumu ya uwekezaji.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kwa baadhi ya nchi za Afrika, Bw. Amos Cheptoo pamoja na Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduor, ambapo kesho, Mheshimiwa Dkt. Akinumwi anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zungu Apitishwa Kugombea Unaibu Spika

 


Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamempitisha Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Spika wa Bunge, jijini Dodoma,  Jumanne Februari 8, 2022.

Zungu amepitishwa na wabunge wote wa CCM baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kupitisha jina lake pekee kati ya wabunge 11 wa chama hicho waliokuwa wakiomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.